Now Reading
“Mawimbi Ya Mwisho” by Ivor W. Hartmann (translated by Okwiri Oduor)

“Mawimbi Ya Mwisho” by Ivor W. Hartmann (translated by Okwiri Oduor)

Last Wave


Mwanaakiolojia Trom Thunbuld alibonyeza kitufu kwenye skrini na kusitisha faili lililokuwa likicheza. Huku akiwa katika hali ya mshangao, alijilaza kwenye kiti chake. Alielekeza macho yake nje ya dirisha, kwenye ufuko wenye changarawe uliokuwa mbali chini yake. Ufuko huo ulimulikwa kwa mwangaza mweupe uliotokana na mapovu ya mawimbi. Alitazama mawimbi haya, huku akishangaa kama huenda bamvua lingekuepo usiku huo. Kana kwamba kwa kufuata kidokezi chake, mwezi ulitua, huku mwangaza wake—mchanganyiko wa rangi za kijani na buluu— uking’aa baharini. Mandhari haya hayakumtuliza kama ilivyokuwa kawaida, kwani maneno aliyokuwa amesikia yalimsikitisha:

Jina langu ni Hamadziripi, nami ni binadamu wa mwisho. Pombooni wananisaka. Washazipata nyayo zangu, na muda si muda watanipata mimi mwenyewe. Siwezi kuepuka yatakayojiri, ila tu ninaposubiri, pengine ni heri kwangu kutoa taarifa hii kama kumbukumbu ya siku za mwisho za binadamu.

Msikilizaji, hongera! Umefaulu tulikofeli sisi. Huenda waelewa fika kuwa kidole kimoja hakivunji chawa, na kuwa azma za uhai ni za masafa marefu. Binadamu hawakuwa wepesi wa kuelewa haya. Kitambo tugundue changamano na udhaifu wa kanuni zilizohimili uhai wetu, muda ulikuwa ushatupa kisogo.

Trom aliwaza kuhusu vipokezi vilivyoegeshwa katika umbali wa takriban light year 47317. Kila moja ya vipokezi hivyo ilikuwa na vijiwaya vilivyotawanyika angani kama wavu wa kumkamata samaki aliye mkubwa mithili ya sayari. Ilieenezwa kwa umakinifu ili ipate kupokea mawimbi mazee, madhaifu na spesheli ya redio. Vipokezi hivi vyenye miundo tata vilihitaji miaka hamsini ili kuunda, na baada ya kuvieneza angani, vikanyamaza ji kwa muda wa miaka thelathini na mbili zaidi. Hatimaye viliweza kunasa mawimbi ya kwanza yaliyokuwa na nishati za kutosha ili kupenya angahewa ya dunia na kusafiri kwa kasi ya mwanga.

Taarifa zilipoanza kumiminika, wote walishangilia. Mwanzoni, taarifa hizi zilikuwa nadra, kisha zikabubujika kwa vishindo. Trom na kikoa chake basi wakaanza kuchekecha na kutenganisha habari hizo. Kazi hii ilichukua miaka mia mbili kukamilisha, na ilikuwa ndiyo sifa bainifu sana ya maisha ya Trom. Kazi hii sasa ilikuwa karibu kufikia kikomo. Trom alishusha pumzi, huku bado akiwa ameelekeza macho yake nje ya dirisha. Alibonyeza kitufu na kuchezesha nakala.

“Sisi binadamu tulikuwa wapumbavu na wenye majigambo. Tulikuwa wabadhirifu kwa matumizi ya rasilimali zetu. Ole wetu, tulizaliwa watoto wa ukahaba, mateka wa mfumo wa kiuchumi uliokuwa chini ya ukatili wa asilimia moja tu ya binadamu wote. Matokeo ya vitendo vyetu yalipoibuka, ilikuwa dhahiri shahiri kuwa tumekithiri taratibu za kiikolojia—”

Hapa, sauti nyororo ya automata ya Trom ilidokeza, “Taarifa katika mawimbi zitakoma kwenye ukadirio wa 10, 25, 08, 0951. Sehemu inayofuatia imedokezwa.”

Mbalamwezi ilitapakaa ofisini mwa Trom na kwenye uso wake pia, akaonekana kana kwamba yeye alikuwa sanamu ilioundwa kwa shaba. Huku akitazama mistarimistari iliyoashiria mawimbi ya sauti kwenye skrini yake, Trom alisogeza kiti chake nyuma, akaketi sasa akiwa ametazama dirisha. Aliangalia nje.

Chini ya pambapamba za mawingu, Trom aliona mashiti ya kijani na buluu yaliyozingia ardhi. Yalizingira vijilima vyenye vilele vya theluji. Trom aliwahi kuzuru eneo hilo lenye mbuga zilizositawi. Aliwahi kufumbata ardhi hiyo nyeusi na kuogelea kwenye maziwa hayo ya maji baridi.

Polepole, mwezi ulipinduka, ukazindua uso uliojaa kunyanzi. Trom sasa akaweza kuona vilele virefu vya mlima Artobus, mlima ambao asili yake ilikuwa mvua wa vimondo.

Trom alikuwa amechoka. Kwa muda wa miaka mia nne sasa, hakufanya chochote kingine isipokuwa kazi hii: tangu kipindi cha ubunifu hadi unasaji wa mawimbi ya kwanza yaliowastaajabisha na kuwasisimua wote. Yote aliyojua kuhusu enzi za binadamu yalimdhoofisha. Alishangaa kama kusudi la uhai wa binadamu lilikuwa tu kutoa nishati za haidrokaboni zilizokuwa zimenaswa ardhini, kwani muda mfupi baadaye, enzi yao ilikamilika. Alikumbwa na huzuni kwani binadamu walikuwa wametia bidii sana lakini hatimaye wakashindwa kulenga shabaha.

Trom aliingiwa na hamu kubwa ya kuona uso wa huyo binadamu wa mwisho, hivyo basi alitazama skrini na kudokeza, “Tafadhali anzisha kisio cha wajihi wa msemaji kutoka kwa ishara zote tulizowahi kupokea.”

“Makadirio yashaanza kutekelezwa. Wataka nikueleze pindi tu nakala itakapokamilika?”

“Ndio,” Trom alijibu. Hakuwa tayari kuendelea kusikiliza habari zile, hivyo basi akaamua kusubiri nakala hiyo.

Ilikuwa vigumu kwake kuamini kuwa kazi hii sasa ilikuwa ikielekea kimiani. Vipokezi vilikuwa vishanasa mawimbi yote, na sasa vilikuwa vimenyamaa kabisa. Yeye mwenyewe alikuwa karibu amalize kuchekecha mawimbi yote. Bila shaka, bado kulikuwa na kazi ya ziada, lakini ya msingi alikuwa ashakamilisha. Kwa kuwa kazi hii ilikuwa sifa bainifu ya Trom, jina lake halingewahi kusahaulika kwenye historia ya spishi yake.

Trom alijilaza kwenye kiti chake, akaelekeza macho yake nje ya dirisha na kutazama mawimbi, upepo na changarawe nyeusi.

“Nakala imekamilika.”

Trom alitazama skrini tena. Alibonyeza kitufu cha nakala na kufumbua picha iliokuwa bila shaka wajihi wa binadamu.

Yu pale Hamadziripi! Macho yake yalikuwa makubwa na yenye rangi ya kahawia. Vigubiko vya macho yake vilikuwa vizito. Nyusi zake zilikuwa kama vichaka usoni mwake, huku pua lake likiwa lenye ncha kali. Kwenye kichwa chake, alifuga nywele timtimu. Uso wake ulikuwa pana na wa umbo wa mraba. Ulikuwa pia umenyauka, na wenye rangi ya kahawia.

“Picha hii ina uhakika gani?”

“Asilimia themanini na nne nukta tano.”

Trom aliutazama uso wa Hamadziripi. “Tafadhali patanisha picha na sauti,” akasema.

Uso wa Hamadziripi ukabadilika, ikawa sasa anatabasamu kidogo. Tabasamu yake ilikuwa dhaifu. Uso wake ulionyesha hisia za hadhari na busara. Trom alibonyeza kitufu kwenye skrini.

Hamadziripi alikuna kidevu chake. Ncha za vidole vyake zilikuwa zenye sagamba. Alitazama chini, huku macho yake yakiwa yamekunjikana kana kwamba alicheshwa na jambo fulani. Muda mfupi baadaye, akainua kichwa chake tena.

“Hapo kale, mja fulani alinieleza kuwa ni watu wanyenyekevu ambao watarithi dunia. Nilikubaliana naye: ndiyo, penye nasibu, wangerithi makaburi yao wenyewe. Mie nishasikia hadithi za masaibu yaliyowapata wanyenyekevu hao. Wao walikuwa kama kurumbiza walionaswa, ila tu tundu walimofungiwa ndani zilikuwa machimbo ya makaa. Mle ndani, idadi ya wafu ilifika mamilioni. Lakini huenda pia uharibifu wa mazingira ulichangia maafa haya yote.

Uso wa Hamadziripi ulibadilika, akaonekana kana kwamba amepoteza hisia. Muda mfupi baadaye, alitikisa kichwa na kuendelea kuzungumza. Alisema, “Si kweli kuwa viumbehai vyote vingine duniani ni hafifu. Kiukweli, viumbehai hivi vina ushindani mkali. Pia, vina uwezo wa kunyakua kwa ukatili nafasi zote ambazo hujitokeza mbele zao. Viumbehai hivi huota kote: si kwenye nyufa za mvuke ndani ya volkano zilizopo chini ya maji, si kwenye ncha za dunia katika vilele vyenye halijoto ya chini kabisa. Nimejifunza kuwa binadamu ndiye kiumbe hafifu wa viumbe na viumbehai vyote.”

Uso wa Hamadziripi ulionyesha uchungu, huku machozi yakijaa machoni mwake. Trom alisikia kishindo kwa umbali.

“Nakala yakoma katika ukadirio wa 20, 45, 15, 0951. Nimeelekeza sehemu ifuatayo. Niambatishe picha kwa sauti?”

Kwenye skrini, uso wa Hamadziripi ulikwama. Ulikuwa wenye huzuni mwingi.

“Ndio,” Trom alijibu. Uso wa Hamadziripi ulimsikitisha, na hakuwa na hamu tena ya kuutazama.

Ghafla, uso wa Hamadziripi ukabadilika tena, ukawa hauonyeshi hisia zozote. Muda mfupi baadaye, akatabasamu, japo macho yake yalionyesha hadhari. Trom alibonyeza kitufu, na faili ikaanza kucheza tena.

“Wacha nikueleze jinsi maafa yetu yalivyotokea. Katika majira ya joto mnamo mwaka wa 2015, hakukuwa na theluji yoyote kule Akitiki, na kiwango cha maji baharini kilikuwa kimepanda kwa sentimita thelathini tangu mwaka wa 2008. Miaka kumi tu baadaye, theluji yote kule Akitiki na Greenland pia ilikuwa ishayeyuka. Mnamo mwaka wa 2008, kabati la barafu la kontinenti kule Greenland lilikuwa na takriban kilomita 3,000,0003 ilhali miaka kumi tu baadaye, wingi wa barafu hiyo ilikuwa ishayeyuka. Kitambo majira ya joto ya mwaka wa 2018 yaishe, kiwango cha maji baharini kilikuwa kimepanda kwa mita ishirini zaidi na kusababisha dhoruba za nishati za ajabu. Dhoruba hizi hazikuwa rahisi kutabiri, na zilizua vurumai kuu mabarani.

Mnamo mwaka wa 2018, ilibainika kuwa ni nyuzi nne nukta moja tu zaidi ya kiwango cha halijoto iliokuwa duniani kabla ya nyakati za ujenzi wa vivanda iliohitajika kufanikisha janga la kimazingira duniani kote. Mnamo mwaka wa 2025, shiti la barafu la Antaktiki magharibi lilitumbukia ndani ya bahari za Ross na Amundsen na kuyeyuka. Mfumo wa kiikolojia basi ukaporomoka, na wengi wakaangamia. Walionusurika kifo nao walichomwa na miale mikali ya jua, kwani tabaka ozoni lilififia kutokana na kiwango kikubwa cha gesi ya methani.

Pombooni ni mojawapo ya viumbe na viumbehai vipya vilivyoibuka kutokana na hali hii mbaya. Au pengine ni sahihi zaidi kusema kuwa pombooni ni mojawapo ya viumbe na viumbehai vilivyojigeuza kutokana na hali hii mbaya. Vizazi saba tu baadaye, Pombooni hawakuwa na budi kukwepa maji mabababuzi ya bahari. Jeni zao ziligeuka, nao wakawa sasa mashujaa walioweza kuhimili ulimwengu huu mpya.

“Sitisha,” alimaka Trom, huku akiwaza kuhusu yale aliyokuwa amesikia. Huenda ikawa pombooni waliibuka kutoka kwa pomboonide ambao kwa upande wao waliibuka kutoka kwa pomboo?

Majibu ya maswali haya bila shaka yangezua utata katika jamii ya pomboo, au kwa jina ya kitaksonomia Tursiops truncatus. Trom alishangaa kama pombooni waliibuka kutoka kwa pomboo jinsi vile binadamu waliibuka kutoka kwa Kenyanthropus platyops. Alishangaa pia kama mababu zake ndio waliokuwa wametekeleza maafa ya binadamu wote walioweza kuponea uharibifu wa mazingira. Wakati huu wote, Trom alidhani kuwa jina la pombooni ambalo Hamadziripi alitaja mara kwa mara katika nakala yake lilikuwa tu ni lakabu mojawapo ya spishi zilizojigeuza ili kuhimili hali mpya ya dunia.

Huku fadhaa ikimpanda, Trom alijitazama kwenye kioo cha dirisha. Jadi yake ya pomboo ilikuwa bayana kwenye ukubwa wa fuvu la kichwa chake, kwenye macho yake mapana na meusi na kwenye mboni zake zilizokuwa na umbo la viatu vya farasi, na pia kwenye pua lake jembamba lililoyeyuka na kuwa tabasamu kwenye mfupa wake wa taya. Trom alipapasa kipulizo chake kwa kutumia vidole vyake vitatu na gumba. Kipulizo hiki chenye manyoyamanyoya kilikuwa nyuma ya kichwa chake. Kiukweli, Trom aliwaza, alifanana kidogo na binadamu. Mlandano huu ulibainika kwenye viungo vyake vinne vilivyokuwa na vidole vinne kila moja, na pia kwenye ngozi yake iliokuwa ngumu na yenye rangi ya kijivu.

Ghafla, Trom akapata wazo fulani. Huenda ikawa ilikuwa ni binadamu waliofanikisha kuponea kwa spishi yake? Binadamu walisababisha janga la kimazingira, na spishi yake Trom iliibuka kutokana na janga hili, kwani iliwabidi kuepa maji na kumiliki ardhi miaka milioni tano iliopita. Bila shaka, matendo ya binadamu yalisababisha kuibuka kwa mababu zake Trom, na hatimaye, mababu zake Trom waliwaangamiza binadamu.

Lakini, Trom aliendelea kuwaza, haya yote hayakumaanisha kuwa binadamu walikuwa waathiriwa hohehahe. Kilichojiri kilikuwa tu swala la mwenye nguvu mpishe, na kama wangepata nafasi, binadamu wangeonyesha ukatili ule ule pia. Hakukuwa na ishara zozote zilizoeleza kuwa binadamu wangeweza kustahimili kuwepo kwa spishi zingine zilizokuwa na busara na taaluma kama zao, kwani spishi hizi zingekuwa washindani wao. Trom hakuwa na shaka kuhusu jambo hili: ukatili wa binadamu haukuwa na kifani. Wakati mwingine, binadamu walipigana na kusababisha maafa wenyewe kwa wenyewe.

Trom aliwaza sasa kuhusu vita baina ya spishi yake na binadamu miaka milioni tano iliopita. Vita hizi ziliashiria mwisho wa binadamu na historia yao fupi, na wakati huo huo, mwanzo wa pomboonide na enzi zao zenye fanaka.

Trom alitazama nje ya dirisha. Angani, mwezi na nyota ziling’aa. Mlima Artobus, au Montes Cacasus kama binadamu walivyouita, uliweza kuonekana. Trom aliwaza kuhusu baadhi ya sifa za binadamu zilizomvutia yeye. Mojawapo ilikuwa kasi ambayo waliweza kustaarabika: kwa muda wa miaka elfu nane tu, binadamu walisonga kutoka kipindi chao cha kwanza cha kustaarabika mpaka kwa safari yao kwenye mwezi, jambo ambalo liliichukuwa spishi yake Trom miaka elfu arobaini kufanikisha. Hatimaye, binadamu waliangamia kwani hawakuwahi kung’amua kuwa mategemeano baina ya viumbehai yalikuwa sharti kwa uhai wote duniani.

“Chezesha,” Trom alisema, huku macho yake yakiwa bado yameelekezwa baharini.

“Siwezi kuamini kuwa makala haya huenda yakawa ishara ya mwisho kuwa binadamu waliwahi kuishi duniani. Mimi mwenyewe sikufikiri kuwa ningekuwa binadamu wa mwisho. Nimetembea pembe zote za dunia nikinuia kuwapata wengine lakini sijafanikiwa. Huenda natapatapa gizani tu, lakini nimeona ni bora kutuma makala haya kule nje kwani pengine siku moja kiumbe fulani kitapata kusikiliza maneno haya. Niwie radhi, usiku huu moyo wangu una uzito. Pia, nimekunywa chupa changu cha mwisho cha wiski ya kimea.

Pokeeni buriani zetu. Nishati zimepungua mno kwenye kituo cha pekee cha setilaiti. Ninasambaza makala haya kwa kwa redio dogo cha HAM kinachopata nguvu kutoka kwa miale ya jua. Kituo cha setilaiti nacho kinapata nguvu zake kutoka kwa tanuri nyuklia lililojengwa zama za kale. Sikudhani kuwa yangehimili yote yaliyofanyika.

“Nina uchovu mwingi. Tangu kuzaliwa kwangu, nimekuwa mpiganaji katika vita. Nimeshuhudia kifo cha wapendwa wangu wote, na hatimaye, kifo cha spishi yangu pia. Pengine wazazi wangu walitabiri haya yote waliponiita mimi Hamadziripi. Jina hii kwa Kishona, lugha yangu ya mama, yamaanisha, “Kila mtu amekwenda wapi?

“Pombooni wananisaka. Hapo awali, niliona nyayo zao. Wana shauku kubwa ya kunipata, na huwa hawasalimu amri mpaka watimize azma yao.

“Maneno ya mwisho ya binadamu yamo mdomoni mwangu. Sijui nikueleze nini. Pengine kuwa wapaswa kutafuta uzuri wa kila kitu? Pengine kuwa wapaswa kuishi kwa upatanifu na mazingira yako? La, naona kuwa cha muhimu kwako kukumbuka ni kuwa—”

“Nakala imekwisha. Naambatanisha faili ATT034, twalijenga tena upya baada ya kukecheka. Nifungue faili?”

“Ndiyo,” Trom alisema.

Mawimbi yalipotea kwenye kimbunga, nayo nakala ikajikwaruzakwaruza halafu ikakwama. Trom alipinduka na kusogeza kichwa chake karibu na skrini. Alisikia sauti ya kuhemahema. Kisha, alisikia sauti za milipuko, naye akagutuka. Ijapokuwa masikio yake yaliwangwa, Trom aliweza kusikia vyema Hamadziripi aliponena, “Basi njooni nyinyi machizi!”

“Faili ATT034 ishafika mwisho. Hakuna taarifa zaidi.”

Trom, ambaye alikuwa katika hali ya mshtuko, alijilaza nyuma kwenye kiti chake. Moyo wake ukigogota kifuani mwake. Mbele yake, picha ya Hamadziripi iliganda kwenye skrini, kana kwamba alikuwa kisukuku kilichohifadhiwa milele kwenye utomvu.


Okwiri Oduor was born in Nairobi, Kenya. Her short story, My Father’s Head, won both the 2013 Short Story Day Africa Feast, Famine and Potluck story contest and the 2014 Caine Prize for African Writing. Her work has appeared in various journals and anthologies in Africa, the United Kingdom and America. She has taken up fellowships at the Macdowell Colony in New Hampshire and the OMI Ledig House in New York. She is currently at work on her debut novel.


Ivor W. Hartmann is a Zimbabwean writer, editor, publisher, visual artist, and author of Mr. Goop (Vivlia, 2010). He was nominated for the UMA Award (‘Earth Rise’, 2009), awarded The Golden Baobab Prize (‘Mr. Goop’, 2009), finalist for the Yvonne Vera Award (‘A Mouse Amongst Men’, 2011), and selected for The 20 in Twenty: The Best Short Stories of South Africa’s Democracy (A Mouse Amongst Men, July 2014). His writing has appeared in African Writing Magazine, Wordsetc, Munyori Literary Journal, Something Wicked, The Apex Book of World SF V2, Litro, and other publications. He runs the StoryTime micro-press, publisher of the African Roar annual anthologies and AfroSF, and is on the advisory board of Writers International Network Zimbabwe.

What's Your Reaction?
Excited
0
Happy
0
In Love
0
Not Sure
0
Silly
0
Scroll To Top