Now Reading
“Somo la Chumvi na Asali” na Mohamed Yunus Rafiq

“Somo la Chumvi na Asali” na Mohamed Yunus Rafiq

F21 saltandhoney


Baba mmoja aliyekuwa na mvi mithili ya majivu ya mti wa mpingo na ngozi iliyokunjamana kama majani ya iliki, aliamua kununua mbuzi katika gulio ili aweze kuwafundisha wanae waliokuwa mabarobaro. Busara zao zilikuwa zimepanda kutoka miguuni kuelekea vichwani mwao. Baba huyo alimchagua mbuzi mweusi kama mkaa mwenye mapembe yenye mikunjo kama mwezi mchanga. Mbuzi yule alimfuata yule mnunuzi kwa kusitasita, kamba shingoni akivutwa kuelekea nyumbani. Mapembe yake yenye ncha yalitawanya vichaka vilivyokuwa katika upande wa njia yenye matope. Baadhi ya siku, pembe za mwezi mchanga huonekana kama vile umekita uso wa anga iliyonywea.

Si kwamba tu aliwashirikisha watoto wake mapenzi yake yote juu ya ule utamu wa maneno na ungwadu wa vitendo lakini alijihimu ili kuwafanya wanae waelewe umuhimu wa vyakula hivi vya msingi katika maisha. Baba huyo mwenye macho yaliyo tulivu, shwari na umri usiosogea kama jiwe lililochongwa aliamuru vyakula hivi viwili vya maisha viandaliwe vizuri. Mikono yake iliyokuwa inaelewa mirindimbo ya maisha – vilio vyake, masikitiko na kukata tamaa, matamanio na makosa, ilimwezesha kuwasilisha maswali ya kwanini na nini umuhimu wa chumvi na asali katika maisha.

Leo hii, kwa msaada wa mbuzi aliyemnunua, mzee huyo alitaka kuona ni kwa kiwango gani watoto wake walifahamu umuhimu wa chumvi na asali na vipi wanaweza kuunga mchuzi wao wa matendo na misukosuko ya maisha.

Mzee yule alimwelekeza mbuzi wake machinjioni, kwenye majani marefu ya chanikiwiti ambayo ncha zake zilikuwa na alama ya asili zilizoshuhudia vifo vya mbuzi waliopita kabla yake. Ni dhahiri, kipande hiki cha ardhi tukufu kilishiba uhai wa mbuzi wengi.

Kwa nguvu na haraka kama kipanga, yule mzee alipokea maisha ya mbuzi yakiwa yanabubujika kama maji na kutiririka katika ubichi wa ardhi. Na ardhi nayo kama buibui anavyofinyanga windo lake ilinyonya ile damu.

Basi, mzee huyo aliwaita watoto wake mabarobaro na wenye hekima vichwani mwao. Alimuuliza kifungua mimba, “Kama nikikupa kipande kizuri cha nyama ya mbuzi, utakila vipi?” Kifungua mimba alisema, “Baba, nitakula nyama yote na kuiacha mifupa misafi kabisa.”

Kifungua mimba aliendelea: “Kama mkulima anapopanda mbegu ardhini, na zao lolote litakaloota liwe hindi au chochote, mwisho atavuna ambacho amewekeza muda wake na nguvu zake katika hilo.”

“Safi sana,” baba yake alijibu.

Baba alimgeukia mtoto wake wa pili, yule mwenye nywele zilizojikunja mithili ya minyoo. Alimuuliza swali lilelile ambalo alimuuliza mwanae wa kwanza. Na hivi ndivyo alivyojibu, “Nitanyofoa nyama zote, kuilamba kila nukta na kuiacha mifupa ikiwa myeupe kama mchana wa jua kali.”

Mwenye nywele za minyoo aliendelea, “Kama mkulima mwangalifu anapoandaa ardhi na kuhakikisha imeondokana na kila aina ya magugu kabla ya kupanda mbegu, nitauandaa mfupa kama mkulima anayeandaa shamba.”

Mzee alionyesha misuli usoni kama aliyetambaliwa na nyoka wadogo huku akitabasamu; tabasamu lake lilikuwa kama radi za mvua kusi.

Yule Mzee alimgeukia mwanae wa mwisho, kitinda mimba. Mawazo ya mtoto huyu yalizunguka kama mawingu, alikuwa na wasiwasi kwamba kaka zake walishasema yote ambayo alitegemea kuyazungumza. Mwisho, mawazo yake yalijipanga kama sisimizi wekundu wenye utayari wa kushambulia na alianza, “Nitaguguna kila chembe ya nyama, mifupa, misuli, mafuta na kamba kamba zozote na kunyofoa kila kilichoambata na mfupa. Huo mfupa utakuwa kama vile haukuwa kamwe umevikwa na nyama. Nitaudhibiti huo mfupa ili unipe kaida yangu na kunishukuru kwa somo la chumvi na asali. Nitauimbia wimbo wa huzuni mfupa huo. Na wimbo huo utauambia mfupa:

     Mgumu wa ugumu
     Onyesha ulaini wako kwake
     Anayekuimbia kwa shukrani
     Kwa tembo
     Kwa kibuyu cha siri ya mapenzi na ujuzi
     Huyu anayekughania
     Siku moja atakuwa kama wewe
     Kuwa laini, kubali kushindwa leo
     Maana nitakuwa kama wewe kesho

Halafu wakati mfupa ukigandamizwa dhidi ya uso wa jiwe la kale katika hali ya kusagwa, jiwe litalipuka kwa wimbo kumjibu kitinda mimba.

     Ewe kitinda mimba
     Ee mtoa shukurani
     Endelea kusagasaga endelea kusagasaga
     Ingawa naweza kuwa mbishi
     Bado nimenyenyekea kwa ndovu
     Yeye ambaye ametujaza
     Kwa siri za vumbi
     Na mawingu

Mpaka hapo mfupa utakuwa mweupe mno, msafi na wenye kung’aa kama kioo. Utakuwa upo tayari kusagwa na kuwa unga ambao nitauchemsha na kuufanya supu kisha nitaukausha kuwa machicha kupunguza njaa yangu. Nitalala kwa shibe na kuota njozi ya mamba wa vina virefu, taswira za mifupa ya mbuzi ambaye baba yetu amemchinja kwaajili yetu kula kwa chumvi na asali.

Kwa miaka mingi, mapepo ya kukata tamaa yalimtafuna ndani mzee huyu lakini jibu la mwanae lilipoteza machungu hayo papo hapo. Alijiona katika macho ya fikra zake akitembea kwa taadhima na kwa yakini kama mwanamke aliyebeba mkungu wa ndizi akielekea gulioni kwenda kuuza zao lake azizi. Alikaa hivyo, aliyezama katika mawazo wakati jua likisogea katika kingo za dunia.

Read the English version “The Lessons of Salt and Honey” by Mohammed Yunus


Mohamed Yunus Rafiq ni mwandishi wa Kitanzania na mtengenezaji wa filamu halisia. Kabla ya kazi zake za fasihi na utengenezaji filamu, alifanya kazi kwenye nyanja ya maendeleo na masuala ya vijana kwa takriban miaka kumi. Yeye pia ni mwandishi shiriki wa mkusanyiko wa mashairi uitwao Mazingira ya Roho na pia anaandika riwaya yake ya kwanza kwa kiswahili na kiingereza. Rafiq ni mwanafunzi wa shahada ya juu ya Anthropologia kutoka chuo kikuu cha Brown. Kwa sasa anaishi Bagamoyo pamoja na familia yake.

What's Your Reaction?
Excited
0
Happy
0
In Love
0
Not Sure
0
Silly
0
Scroll To Top
%d bloggers like this: