Now Reading
“Farah Aideed Aenda Vita Vya Ghuba” na Mehul Gohil

“Farah Aideed Aenda Vita Vya Ghuba” na Mehul Gohil

F15-farahaideed


Translated by Barbara Wanjala

Kurasa za Mein Kampf zimezeeka. Zina madoa ya rangi ya njano na kuna alama za zambarau kwenye maneno yaliyomo. Mifupa ya mgongo wake imeathirika na mikanda ya selotepu inashikilia kila kitu pamoja. Ninaenda kukisoma kitabu hiki mvukeni mwa bafu.

Bafuni mwangu yumo Tabitha, amekaa.

Asema hivi, “Ulitembea hatua chache mbele yangu, kana kwamba mimi si wako wala wewe wangu. Kama watu wasiojuana. Ulitembea kando ukijaribu kunihepa. Daima kuna umbali kati yetu, urefu wa mkono. Kila mara shati lako li mbali na ncha ya vidole vyangu.”

Tabitha yu uchi, mtulivu na mtamu baada ya kulungula, mwili wake nyama zabuni ya paa iliyovamiwa na simba wa njaa aliyekuwa nyege zangu. Tulipendana kwa muda mrefu jana usiku, mashairi ya musosi. Miguu yake ina misuli na chuchu zake ni za furaha. Ana mwili wa mKikuyu ulioumbika Kimaasai.

“Unaogopa. Wewe bado ni pandre tu, mwoga asiyeweza kunikumbatia mbele ya watu wako.”

Anapozungumza nazidi kusoma. Sura ya Hitler kuhusu ‘Asili na Watu’: “Kuna baadhi ya kweli zionekanazo hadharani kwenye barabara ya maisha … lakini, kwa sababu ya udhahiri wao, wengi huzipuuza kweli hizo. Hata mtazamo wa juu juu unatosha kuonyesha … mtu anaweza kuiita sheria ya ulimwengu – ambayo inavifanya viumbe vya aina mbalimbali kukaa ndani ya mipaka ya uhakika ya kiaina wakati wa kujieneza … Panya huishi tu na panya, chiriku kwa chiriku, korongo kwa korongo. Aliyezaliwa mdhaifu tu ndiye anaweza kuona kanuni hii kuwa ya kikatili.

Nakiweka kitabu chini.

“Kweli. Sijui cha kufanya wakati jambo kama hili litendekapo. Mimi hugeuka na kuwa barafu. Nahisi nitajiua kijamii. Nataka kuwa gaidi wa aina fulani, gaidi wa kijamii na kiutamaduni. Gaidi mwenye hisia kali na mwenye kutojali. Siwezi kufanya hivyo Tabitha. Labda siku moja. Sijui.”

“Yule msichana tuliyeona ni jasiri kuliko wewe. Ulimwitaje? Show-stopper? Yule mwenye mvuto mkubwa.”

“Nataka kuyalipua majengo. Nataka kuwaathiri watazamaji watuangaliao tushikanapo mikono. ”

Tabitha auinua mguu, povu ya sabuni yatiririka gotini na mguuni; kisha auleta chini, ndani ya maji, na anikanyaga kwa upole kwenye sehemu ya siri.

“Hivi una matarajio ya kuwa gaidi wa kiasili na kitamaduni, yote kwa ajili ya mapenzi? Huu ni mwanzo, kwa sababu yote yaliyopo kati yetu sasa hivi ni hizi nilizokanyaga, koko zako na Farah Aideed yako.”

Ningependa kudai kwamba mjadala huu bafuni unatokea sasa hivi. Lakini ninaota. Nimekaa pekee yangu ndani ya bafu.

Ni kweli kuwa Bibilia ya waNazi ipo mikononi mwangu, msalaba mwekundu wa swastika kwenye toleo hili la Agosti 1939, toleo halisi lililochapishwa na Third Reich, tarehe ya Agosti mwezi mmoja tu kabla ya mwanzo wa Vita Kuu ya Pili, kama vile ni kweli kuwa kumbukumbu hii yangu ya kikatili ni kukumbuka kwangu kwa Tabitha kwa mwisho. Kumbukumbu ya bafuni kilikuwa kitu cha halisi. Kitu cha halisi cha mwisho.

Nakumbuka jinsi skrini ilivyobadilika kama chembe hadi ikawa nyeupe. Ghafla kituo kikakosekana. Bado mimi huwaza mionzi ya jadi hiyo: Je, alijua yatakayojiri? Je, ilichoma? Je, katika vijisekunde, alipata kuona ngozi yake ikiyeyuka? Je, alipofuka? Je, alihisi hofu? Je, alinihesabu kati ya wapendwa wake?

Nilikutana na Tabitha mara ya kwanza katika matumbo ya jiji la Nairobi ambapo ndani ya hatua za densi za kuvivuka vivuko-milia na wenzangu waliovaa kikoi kutoka Banana Box, suruali za aina ya jeans kutoka Garissa Lodge na vijisuti vidogo vya nyekundu, magari yanapofinyilia breki kwenye ncha ya kivuko-milia, Nissan zipindapo kwa haraka karibu na sketi za cash-and-carry, wakihepa densi na kuingia fujo ya maghorofa yaliyotanda, njia za miguu ambapo mimi huogelea kama samaki wa mji katika mkondo wa mawimbi ya wafanyakazi wa ofisi wanaotoka kwenye maduka ya chipsi na bhajia hadi kwa foleni za ATM, sikio langu likipigwa ngumi na kishindo cha sauti ya baa zilizojawa na mechi za ligii kuu, shimo ndani ya njia ya mkato kati ya Biashara Street naTubman Road, nyayo za chokora ndani ya njia hii nyembamba, mavi yaliyooza na kugeuka nyeusi, kisha naingia pango la giza lililo Dev Towers, kwenye lifti yenye milango yafungukayo polepole kisha kujaribu kujifunga tena nifikapo kisha kufunguka kabisa na ninatoka nje, na kuingia kwenya kilabu cha shatranj kiitwacho Checkmates. Ndiye yule amekaa kwenye bodi, akisukuma kitunda, akijaribu kuuza ngome, kichwa chake chenye rasta kikivisha taji nguo zake zilizoshonwa kwa rangi za buluu na manjano, waridi na zambarau, nguo sambamba na zile za juha aliyejivaa kiucheshi. Alionekana mara moja na kwa urahisi.

Tulisoma pamoja utata wa undani wa mchezo chini ya udhamini wa wachezaji shupavu zaidi nchini, ‘Top Dog’ kama wanavyojulikana. Tukasafiri ndani ya dunia yenye rangi ya mikakati ya mchezo: mbinu ya Kasparov, mbinu ya Boleslavsky ya ulinzi wa Kisisili. Kwenye pande tofauti za bodi, chacharika za kwanza za mapenzi na tamaa zikahisika, kuwaza na kuwazua hatua zinajazojiri kulikuwa kufanya mapenzi kimawazo, ningegeuza ngome na mfalme naye angenicheza Kafara ya zawadi ya kiGiriki lakini kwenye mraba wangu wa h7 vidole vingegusana. Kutongozana kwa upole, kama vile kugusana kwa manyoya.

Tulijifunza kurekodi michezo yetu kwenye vijikaratasi vya alama. Ningeandika ‘22.Rd5’ naye angejibu ‘22…Qxd5’. Angeupoteza uzi wa mchezo wake na angeomba wangu ili aboreshe wake. Ningeandika juu ya kijikaratasi chake, “Je, ungependa kuenda sinema saa 2:30 baada ya majaribio yako ya uonyeshaji mitindo?” na angekirudisha na jibu lake. Wachezaji wenzetu waliuona utoto wetu huu wa huku na huko lakini tuliendelea bila aibu.

Niliviweka vijikaratasi vyote. Nikivishikilia sasa mikononi yangu kuvisoma, bunda hili la historia yetu binafsi ni nzito mno.

Hiki ndicho kile ambapo nilimfunga kiMaroczy. Wakati wa uchunguzi wa maiti baada ya mchezo huo, alisimama na kuniuliza kwa nini hivi au vile, mbona hatua hii na wala si ile. Alikiangalia kichwa changu nilipojikunja kwenye bodi, akakiangalia pale ambapo nywele zilikuwa zimeanza kupungua. Kupungua kwa haraka. Kitu kilikuwa kinanitokea na alitaka kujua kitu kipi hasa. Huu ndio wakati nyufa za kwanza kati yetu zilianza kuonekana, nilipokaa kimya na kucheza kizungumkuti ili kuhepa maswali yake. Nikaacha kifagio cha nywele zangu kiwe na kuwa pori, na kilimpendeza.

Tulikuwa mateka katika uzuri na ubatili wa mchezo wetu. Shatranj ilikuwa mithili ya kifaa cha kuturudisha nyumbani na mithili ya madawa ya kulevya. Farasi wangu mweusi hakuwa kamili bila bishofu wake mweupe.

Kisha kuna kijikaratasi hiki cha mwisho kilichoanzisha safari yetu ya mwisho:

Hakuna kitu hapa, wala mbinu, wala jina, hamna kitu. Kuna baadhi tu ya michoro. Nilikuwa nikimsubiri nyumbani mwangu Westlands, nikachora kwenye uso wa kijikaratasi na kalamu.

Akaja, nikakiweka kijikaratasi mfukoni kama ilivyo jinsi yangu na tukaenda kwenye kituo cha matatu.

“Kwa hivyo hizi ndio njia kuu zenye joto za Westlands,” akasema.

Jua la asubuhi liling’aa kupitia nyufa katika vivuli vilivyotupwa na majengo, nyumba, miti na mabango ya Tusker.

“Ongeza watu zaidi na maisha zaidi kwa vijibarabara hivi na tutapata Eastlands,” alisema.

“Eastlands ni kama Bobby Fischer: mlaghai, wazimu na mshenzi, mahali ambapo ukipoteza nafasi yako watafurahia kukuona ukitetemeka,” mimi nikasema.

“Ha! Hujawahi fika huko!”

“Tunaenda huko!”

“Na Westlands ni kama nani?”

“Kama alivyo Vishy Anand, mtu ambaye anakuwacha uzichukue tena hatua yako mbaya, anacheka nawe, na badala ya kukuruhusu ujiuzulu anakuuliza kama ungependa idli sambar na White Cap kadhaa.”

Mawimbi ya trafiki ya asubuhi yalikuwa yaja. Kwenye barabara nyembamba zilizomo kati ya vijibarabara magari yakaja yakisimama kwenye makutano au nyuma ya mistari ya trafiki kwa muda na kisha kuingia kwenye mishipa yalishayo Uhuru Highway na kuelekea kwenye matumbo ya mji.

“Kunileta nyumbani mwako ni tatizo zaidi,” akasema.

“Wewe! ninajaribu!” nikasema.

“Naam, sikuamini.”

“Angalia, mimi huhisi hofu nikiwaona hao matafaka ambao wanafanana nami wakipita ndani ya Toyota na 4WD zao. Si kwa sababu yako. Ni kwa sababu yangu.”

“Ni vizuri kwamba unaweza kujionea pole.”

“Nikiwaona wakiniona nikitembea ninayaona mawazo yao, nawasikia wakifiri: Sina gari kwa sababu siwezi kumudu gari.”

“Ni mantiki.”

“Hapana, kwa sababu baba yangu pengine ni mhasibu afanyaye kazi katika kampuni imilikiwayo na mojawao, na mwanawe ni kama yeye tu.”

Mawimbi ya trafiki yakaongezeka. Magari yakapunguza mwendo. Madereva mumo ndani walionekana kuchoka. Tulipita chini ya bango kubwa la Safaricom.

“Ni kitu gani hasa? Hawa matafaka matajiri waliovaa madigaga, walionyolewa visafi, wanaovuta sigara na kuzungumza kwenye simu rununu walioshika ushukani wanakuwasha?”

“Nasema hivi, nadhani kuwa mle Eastlands naweza kuwa mimi mwenyewe, mimi binafsi,” nikasema.

“Au ni kwa sababu baba yako na mwanawe hamna uwezo wa kufikiria kama Kamlesh Pattni au pandre mwingine yeyote yule?”

Matatu moja ikaja na tukaingia ndani. Ilituchukua mbali na vijibarabara vya miguu wazi.

Nilipenda matatu zangu ziwe kama hii – zivae madigaga. Sikutaka mapandre wenye magari kuangalia ndani zao na kuona uso wangu mweupe uliomulika kama mwangaza mle ndani. Ni kweli kuwa hawangeweza kunitambua isipokuwa kama wangelinijua, lakini wangejua mimi nilikuwa nani hata hivyo. Wasingelijua jina langu, wasingelijua pale ambapo nilipoishi, lakini wangelinijua mimi.

“Unaondoka lini?”

Matatu ikageuka kuingia Kipande Road baada ya kupita Aga Khan Nursery School.

Tulikuwa tukiacha nyuma kitongoji changu – nyumba zilizoshikilia ukale wao na kufichwa nyuma ya milango ya chuma, maua ya aina ya bougainvillea na kuta za zamani. Nyumba zilizofuata mpangilio nadhifu kwenye tawi za barabara nyembamba za Westlands, nyumba hizi pamoja na majengo mafupi yaliyokuwa nyumbani zamani na sasa kugeuzwa ili kupata faida, na maduka makubwa makubwa yaliyosimama ulinzi kwenye kingo za Westlands.

“Siku baada ya kesho,” akajibu.

“Nimekuwa kitunda duni sio?” Nilimuuliza.

“Unaweza kujaribu kunitia moyo siku ya kuzaliwa kwangu. Unaweza kufanya jaribio la mwisho ili kuuokoa urithi wetu.”

“Nitakununulia vitabu unavyopenda.”

Sasa tunaingia Kipande Road, hasa pale ambapo barabara huzama unapoelekea Globe Roundabout. Nyumba nzuri na majengo nadhifu zinageuka kuwa majengo yaliyosambaratika – gereji za barabarani zikikaimu picha zao za uchi, nati zilizosambaa kwenye urefu wa barabara, hosteli za wanawake zenye majina kama “Jupiter Girls Accomodation” ambapo ungeweza ona mambo ya ndani kwa njia ya madirisha – na tena kwenye urefu wa barabara nyumba na majengo na maduka na Hare Krishna Temple zote zimepangwa kwenye matuta yaliyopanda ili kumudu kwa bega uzito wa Ngara nyuma yao.

Jua ilijitupa juu ya urefu wa barabara ikakata kwa vipande vivuli vya mabango; tukatembea tukigeuza joto ya jua na vivuli baridi vya Barclays Bank na Bata Shoes.

“Siendi milele,” akasema.

Matatu ikafika Globe Cinema Roundabout. Kwenye mzunguko magari yaliyopakwa PC World, Keringet, DSTV kwenye miili yao yalibusiana, na matatu zingine ambazo zilileta watu ambao walifanya kazi kwa makampuni haya. Kule Globe ulikuwa mji ambapo Johnny Walker alikuwa amehifadhiwa kama jogoo kwenye maghorofa. Na katikati kulikuwa mto wa Nairobi, mwisho wa mchakato wa mabango – wanaNairobi wakinya vyooni mwao miharo mizima ya Kenylon Baked Beans, wakikojoa susu yao yenye sukari ya Coca Cola na Ketepa, wakisafisha nyuma yao na Harpic ya kusababisha kansa, hii yote ilitiririka mtoni.

Matatu ikatuleta hatimaye mjini.

Tulitembea ili kukamata matatu ya kuunganisha hadi Eastlands na kupita kando ya msikiti wa Jamia ambapo muziki wa maombi wa Ijumaa hiyo ya moto ingetokea na tukaangalia wakati kwenye saa refu za jiji.

Ingekuwa saa 4:23 asubuhi mjini New York na saa 11:23 jioni mjini Nairobi Ijumaa.

Tukapita katikati mwa usafi wa Kimathi Street ambapo skrini kubwa za tangazo za LCD ziliing’arisha na kuipa Nairobi mnato wa wakati ujao na teknokrasia; kila kitu kiling’ara mithili ya picha timilifu, kama ilivyo Times Square, New York.

Kwenye skrini moja ya LCD tuliwaona pandre watatu wakilitazama bango la Nivea kando yake. Mwonyesha mitindo wa kiAfrika akiwa nusu uchi, akionyesha ngozi yake na tabasamu. Nivea. Wanaume hao watatu walionekana kama walio kwenye ndoto.

“Ya Nivea ni homo erectus na hii ya LCD ni homo sapien. Inaonekana kuwa na akili na maisha yake binafsi,” alisema Tabitha.

Matatu ikapita kwenye trafiki ya asubuhi iliyokuwa ikipungua kwenye Jogoo Road. Nilikuwa nikitarajia kabeji zinazooza, nguruwe wanaorandaranda na mapigo ya nzi yaliyotanda kwenye paa za mabati lakini yote niliyoona ilikuwa nyumba na maduka na makanisa na shule bila mwisho, yote haya yalikuwa yamepangwa kwenye mistari moja kwa moja kama majeshi ya Fischer kabla ya hatua ya kwanza. Hakikuwa kitongoji duni, ilikuwa ni Eastlands tu.

Tuliwasili katika Jericho Social Hall na mapatza wa Checkmates wakatusalimu, “Karibuni Urusi!”

Mimi na Tabitha hatungewezana na maTop Dog kwenye mashindano yaliyopangwa. Tulipoteza mchezo baada ya mchezo lakini tulifurahia starehe ya umeme kimya wa anga. Ukumbi wa mashindano ulikuwa mtulivu. Kulikuwa tu na wachezaji waloinamia bodi zao wakitafakari kimonaki. Lakini kimya hiki hakikumaanisha ukosefu wa mawasiliano. Katika kule kucheza mbinu, mabishano makubwa yalitokea. Sisi wanashatranj tulisikia kishindo wakati kafara ya bishofu wawili ilipita kwenye utetezi wa upande wa mfalme. Sauti za “Aaah!” nyororo za watazamaji wachocheaji wakati wa kilele cha Philidor Legacy ulikuwa kama kundi la tembo likivuka daraja la 7.

Machweo ya jua yalianza kujidhihirisha na kila mtu akaingia kwenye milango ya nyuma ya Eastlands. Baada ya kupitia kwenye mabonde yaliyokuwa sawa na mengine yaliyokuwa ya mistari ya sulubu, tulikusanyika sote katika Paradisio Bar. Masifu ya jioni, ambapo povu ya bia za baada ya mashindano ilijaa katika glasi zetu. Msamiati wangu ulichanjwa na maneno mapya, sheng ilikuwa na ladha mno. Tabitha aliona aibu kwa majaribio yangu kuyaongeza maneno haya mapya katika hotuba yangu ya ujumla.

Nilimchukua kando. Midomo yetu ikalainika Tusker ilipoonyesha nusu kwenye glasi. Chupa ya tatu ikamfanya ateleze kiganja chake kwenye kitovu changu na nikaziona taa za Paradisio machoni mwake.

Nikaja kugundua kwamba, mle mwenye jumba la sinema la 20th Century Fox, wakati wa jioni ambapo mlikuwa tupu, licha ya haiba ya Hollywood kwenye skrini, ningeweza kuzivua nguo za Tabitha na kumwacha uchi wa mnyama, ningeshiriki katika kitendo cha kulungula au musosi. Nikagundua kwamba sehemu zangu nyeti wakati huu zilijulikana nyakati hizi kama ocutambula au tu Farah Aideed. Na nikizitoa nje, nazipeleka kwenye Vita Vya Ghuba. Farah Aideed aenda Vita Vya Ghuba, wakati wimbo wa taifa unacheza, Tabitha yu uchi mikononi mwangu. Au kitu kingine tofauti siku nyingine, jioni nyingine, usiku mwingine wa sinema – namvua sidiria na chupi, niko nyuma yake, Farah Aideed kwenye ufa wa matako yake. Ageuza uso wake kunibusu. Nayakamua matiti yake. Anageuka. Mikono yake shingoni mwangu. Nipe nikupe.

Maisha kama haya yanaweza kukuzengua.

“Nimekuwa nikiwaza. Baadhi ya maneno haya yana maana makubwa. Vita ya Ghuba. Hii inaweza kumaanisha uwanja ambapo mtu, Farah Aideed, anaweza kujitambua mwenyewe. Inaweza kumaanisha kugundua mahali ambapo unaweza kuiita nyumbani,” nasema.

“Wewe wakati mwingine hunifanya nisikie nisiondoke,” alisema.

“Lakini utarudi tena.”

“Ninahisi kama sitarudi kamwe.”

“Usiseme hivyo. Simama imara, bado tutakuwa pamoja. Nitakununulia vitabu.”

“Ninadhani sina maana kwako tena.”

“Wajua kwamba wewe ni Vita vyangu vya Ghuba? Si tu kimwili. Wewe uwanja wangu wa michezo, uwanja wenye msimamo mkali. Umenileta nyumbani. Angalia tulipo. Singewahi pajua mahala hapa. Wewe ni vita dhidi ya kile nilichokuwa,” nilisema.

Kukumbatiana kwetu kukafadhaika. Mapatza wa shatranj waliolewa walitaka kuelekea ngazi za mapinduzi. Walitaka kuenda kucheza shatranj Karumaindo. Nilitoa pingamizi, nendeni mtuache.Sikuwa nimempima Tabitha. Nilitaka kupata muda naye kabla aondoke.

Tulifika Karumaindo hivi karibuni. Jumba la uasherati lisilokuwa kama lingine lolote. Mchanganyiko wa msongamano na mataa meupe yaliyomulika mapaja manene na alama za miezi tatu ya mimba kwenye matumbo ya makahaba mamamboga.

Tukachukua bodi na saa zetu na tukacheza kati eneo geni zaidi ya zote. Ilikuwa ajabu kwangu – shatranj ya ligi kubwa ikichezwa katika eneo ya dhambi zaidi nchini usiku gizani. Mamamboga wakakusanyika karibu na meza zetu. Hawakuelewa kamwe kuhusu mbao tulizosukuma juu ya bodi zetu lakini walipiga filimbi kila baada ya hatua na kugusa vipande vilivyotekwa kwa mshangao.

Bia zilimwagika. Nililewa kiasi na kumgusa mamamboga jirani. Tabitha akakasirika papo hapo. Akamchokoza mamamboga na mamamboga wenzake wakaja kumtetea. Matusi ya Kikuyu yaliyofuata yalimfanya Tabitha alie. Akageuka kuondoka. Nikamfuata nyuma.

Nilimpata nje. Alikuwa amepoteza utulivu na akaniambia nipotelee mbali. Potelea mbali. Potelea mbali. Potelea mbali. Umati ukakusanyika karibu nasi. Kwa namna fulani nilimtafutia teksi.

Kugeuka nyuma kuelekea Karumaindo, nikasimamishwa na polisi wawili wenye silaha. Hii haikuwa jambo la kawaida la kitambulisho na rushwa. Walitaka kunichukua ndani ili kunihoji.
Mapema asubuhi iliyofuata, waliniacha huru baada ya kuridhishwa kuwa sikuwa Ahmed Razzaq Abdul, Moiz Khalif Hussein, Razzaq Mousavi au Mushtaq Pervez.

Nikatazama simu yangu na kuona idadi ya ujumbe na simu nilizokosa, zote kutoka Tabitha. SMS hizo ziliumba hadithi yao zenyewe. Nikaelewa kwamba Tabitha alikosana na mamake aliporudi nyumbani. Uhusiano kati yao haukuwa mwema. Hangeweza kubali kuwa mamake alimwona kama aliyeshindwa maishani – alichelewa kurudi nyumbani, kazi isiyo imara, ukosefu wa akiba baina yao wawili. Tabitha akanywa chupa nusu ya Kenya Cane. Mamake akafanya vile vile. Nyumba ya walevi wawili wakitusiana na kuumana. SMS zilizofuata zilikuwa matusi tupu. Mimi hili, mimi lile. Mimi niliyempotosha.

Nikathibitisha kuwa simu ya mwisho niliyokosa ilikuwa tu dakika chache zilizopita. Nikampigia.

Kwa sauti iliyochoka yeye aliniambia, “Je, ulifurahia kuweka Farah Aideed yako ndani ya mojawapo wa mamaboga baada nilipoondoka na kukuwacha kwa amani?”

“Sikukuu njema ya kuzaliwa!” nikasema.

“Ah ndio! Najisikia poa!”

“Nilikamatwa baada ya wewe kuondoka.”

“Kwa sababu ya kunicheza na mwasherati mwenye mimba? Niambie ukweli.”

“La! Walidhani mimi ni gaidi au nina uhusiano wa kigaidi. Walisema ninaonekana na aliye na tuhuma. Walinichukua ndani kunihoji na kuniuliza kuhusu mipango ya al-Qaeda. Hata walinipa kikombe cha kahawa na biskuti. Walitaka nizungumze. Walidhani nina habari kuhusu jambo kubwa litakalotendeka na kwamba nina habari kulihusu.”

“Haya basi. Tuonane Westgate saa sita mchana. Unanipeleka kununua vitabu. Ninastahili baada ya yote uliyonitendea. Hebu tuone utajifanya vipi mbele ya pandre wenzako ukiwa nami.”

Kule Westgate nilifanya makosa yote Tabitha aliyotaja bafuni. Nilipanda kipandishi hatua mbili mbele yake, nikaongeza kasi kisha nikapiga mstari sulubu kwa ghafla kwa sababu nilijua hangeweza kufuata kwa urahisi na viatu vyake vya juu, nikaenda kumsalimia mjomba fulani kwa mikono, halafu nikapita kwenye mahakama ya chakula na kuungana naye tu pale ambapo nilikuwa na uhakika tulikuwa mbali na macho ya mapandre.

Kuelekea mwisho wa safari yetu tulikaa kule Nandos. Sijui kama alikuwa na tatizo na jinsi tulivyoketi, tulikaa tukiangaliana mezani. Sijui kama hiyo ilikuwa sawa. Tulikuwa na vitabu vyetu na kurasa zao zilinukia upya wao.

“Ningependa kukunukulia Castaneda, kama nionavyo, “Mtu mithili ya Farah Aideed hatatanishi vitu. Analenga kuvirahisisha. Anatumia akili zake zote kabla ya kuamua kuviingia Vita vya Ghuba. Kwa vile vita vyovyote vya Ghuba ni vita vya maisha yake. Farah Aideed lazima awe na nia na awe tayari kuchukua msimamo papo hapo,” alisema Tabitha.

“Nadhani nimethibitisha leo kuwa mimi si aina hiyo ya Farah Aideed,” nilisema.

“Sasa wacha nikunulie The God of Small Things ya Arundhati Roy. Hii ni sehemu ambapo mama mkwe anagundua kuwa binti mkwe wake amekuwa akilala na mmoja wa wenyeji, wale waHindi wa kusini weusi, zaidi ni wa kienyeji, zaidi ndio weusi. Wasiwasi wake kuu si aibu kwa hali yake ya jamii itakayotokana na kitendo hiki lakini swali lake kuu ni: vipi ulivumilia harufu yake?”

“Ehe.”

“Huu urafiki wetu ni nini? Mimi ni mpenzi tu au?”

“Eti nini?”

“Nikwambie nini, niambie baadhi ya mambo yaliyomo kichwani mwako sasa hivi, kwa kubahatisha. Mambo yoyote matatu kichwani mwako. Labda nitakuelewa bora namna hiyo. Mambo yoyote matatu, chochote kile, kwa kubahatisha.”

“Haya. Ninawaza kwamba bara la Afrika linasalia nyuma kimaendeleo kwa sababu Waafrika hawana ujuzi katika kuchagua uongozi.Sisi kama WaAfrika tuna akili kama yeyote yule lakini karne hizi zote tumezingatia zaidi uongozi mbaya, fitina za kisiasa na mambo kama haya. Miaka mia yaliyopita WaAfrika wangekuwa wakibuni baruti badala ya kucheza siasa na tungekuwa wakoloni badala ya kutawaliwa na wakoloni.”

Alikuwa akinywa sharubati kupitia mrija na kitendo hiki kilitoa sauti iliyolingana na ya ushuzi. Nikaendelea na wazo langu la pili.

“Matatu ina hewa. Milango yake ni wazi. Unaweza toka nje wakati wowote. Inachukua abiria yeyote wakati wowote. Itakupeleka mahali popote, bora uchukue itakayokupeleka unapotaka kuenda. Gari binafsi linakufunga. Huwezi toka nje hadi ufike unapoenda. Huwezi kuliacha nusu njiani.”

Alikuwa akifurahia sana sharubati yake.

“Westlands Road inaenea kutoka zogo ya China Plate na Chowpaty na inaenda hadi eneo ya zamani ya International Casino. Wakati wa jioni, makahaba na polisi wenye silaha huzuru barabara hii. Mapandre wapitapo barabara hii, magarini mwao bila shaka, mume na mke katika kiti cha mbele, watoto wenye umri mdogo nyuma na mama mkwe mwenye sura mbaya akasirikaye kwa haraka, wao hujifanya kuwa hao Wakenya wa jioni hawapo. Kwa barabara kama hizi, maisha nje ya magari yao ni sayansi ya uongo, kitabu cha Isaac Asimov. Siku moja, kwa mchezo tu, simama popote kwenye Westlands Road na uhesabu mapandre wangapi wanapita. Idadi yao ni siri isiyojulikana nchini Kenya.”

Ninapomaliza kusema hivi anatoa sauti za kunyamba na kinywaji chake.

“Hebu fikiria jinsi ingekuwa kama tungeweza tazama yote yaliyo chini kutoka kilele cha Uhuru Park, maghorofa na yote, yakilipuliwa na bomu ya nyuklia. Tungehisi vipi kuutazama mlipuko huu kiukweli badala ya kwenye sinema au televisheni? Tungeweza kusimama pale na kutazama na kusema itokeapo ‘Nimekuwa kifo, muuaji wa dunia zote.”

Akayatoa midomo yake nyororo kwenye mrija na kuniambia, “Eti nini?”

Kwa dakika chache tulikaa kimya na kumaliza kula kwetu. Kisha akanilenga na macho yake.

“Nadhani nyinyi wanaume wachuti mnataka tu kuma nyeusi.”

“Hapana, hiyo si kweli.”

“Nini mbaya na wasichana wenu wachuti? Mbona huna mmoja?”

“Tatizo la wengi wao ni kuwa hawana uhakika wanachotaka, wamechanganyikiwa.”

“Nadhani ni wewe uliyechanganyikiwa, mawazo yako hayaeleweki. Je, una msichana chuti mahali fulani? Wengi wenu mko hivyo, au siyo?”

“Ningewezaje? Mimi si kitu zaidi ya mtu anayependa kukaa pekee yake, mchezaji shatranj ambaye mawazo yake hayaeleweki. Wasichana mapandre wanapendelea zaidi kunyongwa na hisia za Bollywood ambazo wanaume wanaweza wapa.”

“Sikuelewi hasa. Hivi unasema wasichana wengi wachuti wako hivyo?”

“Labda wote. Inawezekana kunao walio tofauti.”

“Wasichana wachuti wako hivo tu? Na je waliyomo madukani humu sasa hivi?”

“Naam, kuna uwezekano zaidi ya mambo ya aina ya kiFarah Aideed kumtokea msichana pandre kama asingelikuwa pandre sana. Haiwezekani kwa msichana madukani humu, kitongojini humu, kuishi maisha tofauti na yale niliyokueleza. Hata mimi ninaogopa kukumbatia kwa undani katika eneo hili. Ingekuwa kujitia kitanzi.”

Alinisimamisha hapo, ilikuwa wazi kuwa hakufurahia jibu langu.

“Angalia nyuma yako. Nimekuwa nikitazama wapenzi hao wawili tangu walipokuwa katika duka la vitabu. Labda hukuwaona kwa sababu ya upandre wako.”

Akaondoka.

Nikageuka nyuma. Kitu cha kwanza nilichoona kilikuwa mapandre hawa wawili, Mahesh Patel Shah na mkewe Anju Lohana Shah. Mahesh, mrithi wa biashara za babake na pia wa uwezo wake katika jamii ya mapandre. Nikageuza kutazama alipozungumzia Tabitha. Nikafuata macho ya watu. Kila mtu alikuwa akiwatazama.

Kwenye milango ya lifti walisimama msichana mmoja Mkenya mwenye asili ya kihindi. Na hili ndilo lilikuwa show-stopper: alikuwa akimkumbatia Ololo mzuri kutoka ziwani na walikuwa mdomo kwa mdomo.

Waathirika wa kwanza walikuwa wale waliokuwa karibu karibu. Mlipuko uliwatupa mbali kwa ghafla. Sari na kurta zilishika moto. Anju Lohana alikimbia kama paa hadi mlango wa kutoka na Mahesh aligongwa na kijipande cha chuma na damu iliyokuwa ikivuja mwilini mwake ilitaka kumuua.

Kisha wimbi wa mshtuko ukaanza kushuka hadi kwa ghorofa ya kwanza, ghorofa ya chini, wanandoa wale wa ololo sasa wakauchukua uharibifu kwao nje ya maduka hayo. Waathirika walionusurika walikimbia kuelekea eneo za salama katika vitongoji vya Parklands na Westlands vitongoji na baadhi walikuwa wanakwenda nyumba hadi nyumba ili kuonya wote kuhusu pigo lilokuwa karibu kuwasili. Mwisho, maduka ikabaki na miili mingi yenye bongo zilizoaga, waathirika ambao hawakuweza kusajili kile kilichotokea.

Baadaye mimi na Tabitha tulikuwa bafuni. Hiyo ilikuwa ni kama kwaheri yake kwangu. Yeye alikuwa akienda New York siku iliyofuata. Hakunipigia siku aliyoondoka. Kwa kweli, baada ya bafu, hakunipigia tena.

Nilimtumia barua pepe. Nilisubiri jibu. Siku moja, siku mbili, siku ya siku nne…

Ile Ijumaa ya moto akanitumia jibu. Tumaini dogo.

Trafiki ya Ijumaa katikati ya jiji likuwa nyingi zaidi. Joto ya miili ya wanaNairobi ilihisika. Nilipotembea kando ya msikiti wa Jamia utamu wa Kiarabu ya maneno ya Qurani yalijaa hewani. Haikuwa kelele. Ilikuwa takatifu.

Nikawasalimu wachezaji waliokusanyika.

Hii ilikuwa ni Checkmates. Kilabu ya hali ya chini. Televisheni ndogo kona ilionyesha habari za CNN, viti na meza plastiki, baa ilikuwa ndogo na hafifu kujaa bar na harufu ya mkojo ilienea kupitia mlango kuu kutoka vyoo vya jirani.

Nilichukua nafasi yangu kwenye meza ya ‘daraja 4’ na vipande yangu vikapigana vita na vya wapinzani wangu. Ilikuwa Blitz na mimi nilipenda kasi wa kucheza.

Ukumbusho wa Qurani uliendelea wimbo wake wa ndege, unyororo wake ungedhani ungeweza kuona sauti ikiruka juu hewani katikati ya jiji la Nairobi.

Kisha baadhi ya mapatza wakatupa ishara kwetu twende tukatazame televisheni. CNN ilionyesha sehemu ya Times Square mjini New York: mabango ya elektroniki na skrini za ishara na maghorofa yaliyoinyesha kuwa mji mkuu wa fedha duniani. CNN ilionyesha Osama lakini hii ilikuwa tofauti. Alikuwa kwenye idadi ya skrini zilizoenea pote Times Square. Wamarekani walikuwa wamezingira hizi skrini kana kwamba wanaotoa heshima kwa mwimbaji mwenye fani. Osama alikuwa akiongea kwa lugha ya Kiarabu. Hatukujua nini alikuwa akisema. Lakini ya kuvutia zaidi ilikuwa umati wa watu. Walikuwa wakionyesha pande zote kwa vidole. Osama alikuwa kila mahali na pembe kamera hazikuweza kukamata kila kitu.

Tuliangalia nyuso katika umati wa watu ili zituonyeshe nini kilichokuwa kikitokea katika maeneo mengine.

Osama aliendelea kuzungumza kwa dakika chache zaidi, sisi katika Checkmates tulianza kuchoka na tukarudia michezo yetu ya shatranj. Hivyo basi video nyingine ya Osama. Kwa hivyo? Hacker fulani alifaulu kuicheza kila mahali New York. Vyema sana. Turudi kwa mchezo.
Dakika chache baadaye mtu mwingine alituhimiza turudie televisheni. Uso wa Osama uliwekwa kando ya sampuli ya video zilizoonyesha mifano tofauti ya mlipuko wa bomu ya aina ya A. Video ya kihistoria ya Hiroshima. Vipimo vya kiatomiki Nevada. Namna hiyo. Hii ilikuwa ina mvuto kabisa. Kila mtu alikuwa akitazama. Michezo ikasimama. Nini hii?

Ungeweza kuona umati wa watu kwenye CNN wakiwa na tabia tofauti sasa. Wote walionekana kuwa kipaumbele kama kikosi kijeshi. Osama akaendelea kuzungumza. Yote yalikuwa kwenye Kiarabu.

Bomu ya H ikapanuka kama ua juu ya Bikini Atoll, uso wa Osama kama kivuli kwa nyuma.


Barbara Wanjala is a Kenyan writer. She was shortlisted for the 2015 Haller Prize for Development Journalism. Most recently, she has contributed to the African creative non-fiction anthology, Safe House: Explorations in Creative Nonfiction (Dundurn Books, 2016).

Mehul Gohil is an Africa39 writer and a founding member of the JALADA collective. A Don DeLillo fanatic and an MJ disciple. He is also a chess addict and a member of the Kenya national chess team. Born and living in Nairobi.

What's Your Reaction?
Excited
0
Happy
0
In Love
1
Not Sure
0
Silly
0
Scroll To Top