Now Reading
“Kumwasha Babu Moto” Na Neema Komba

“Kumwasha Babu Moto” Na Neema Komba

F19 settingbabuonfire


Ana, kwa nini umejiunguza? Sista Clara, muuguzi mkuu wa shule ya sekondari ya wasichana ya Mt. Maria aliniuliza huku matron wengine wawili wakiwa wameifunga mikono na miguu yangu kitandani.

“Babu aliniambia nimwashe moto,” nilinong’ona, sauti yangu ikitetemeka. “Alisema anataka aisikie miale ya moto ikilamba ngozi yake iliyojaa makunyanzi. Nilipojiangalia kwenye kioo asubuhi ya leo, nilimwona tena; jirani yetu mzee mwenye mapengo na ngozi iliyokunjamana akiwa amejifunika shuka la bluu,” nilimwambia Sista Clara.

Msalaba mkubwa ulining’inia shingoni mwa Sista Clara. Alishusha miwani yake kidogo na kuniangalia kwa ukali kana kwamba macho yake yangeweza kuunguza mzimu wa babu uliokuwa ndani yangu. “Babu hapendi baridi,” nilimwambia Sista Clara lakini hakuniamini. Anafikiri mimi ni mwendawazimu. Kila mtu anafikiri mimi ni chizi, na mwongo.

Nilikumbuka siku ambayo babu alinikuta nikiwa nachochea moto wa kuni kwenye jiko la nje pale nyumbani. Nilikuwa na umri wa miaka kumi. Nyumba yetu ilikuwa ya matofali ya kuchoma yenye mlango na dirisha moja huku ikiwa imeezekwa na nyasi. Kuta zilikuwa nyeusi kwasababu ya moshi wa kuni ambao uliniumiza macho. Nilipanga kuni kwenye mafiga matatu na kupulizia moto ili uwake. Machozi yalinitoka kutokana na moshi uliofuka kwenye kuni. Sikumuona babu alipoingia.

Nilishtushwa na mkono wa babu kwenye bega langu la kulia. Alinikazia macho yake mekundu kwa ukali utadhani nilikuwa nimemkosea kitu. Moyo ulinidunda mbio kwa hofu lakini sikuacha kukoka moto. Babu alinivuta na kunibana katikati ya miguu yake; nilishindwa kufurukuta. Sikuelewa kilichokuwa kinaendelea. Alisema anasikia baridi; alitaka nimpe joto; alitaka miale ya moto iliyo mithili ya ndimi za rangi ya machungwa iguse mikunjo ya ngozi yake iliyozeeka. Aliponigusa kwa vidole vyake nilihisi kuungua moto mithili ya mtu aliyeko jehanamu.

“Niache!” nililia na kuweweseka kwa uchungu, wakati Sista Clara akinidunga sindano ya usingizi. “Shhhh shhhh tulia” alinibembeleza kwa sauti ya upole. Macho yalianza kufumba yenyewe na taratibu nikapotelea kwenye ulimwengu wa usingizi, kila kitu kikiteketea kwa moto mkali.

Read the original story “Setting Babu on Fire” by Neema Komba


Neema Komba ni mshairi na mwandishi kutoka Tanzania. Ni mshindi wa Tuzo za Fasihi za Etisalat katika hadithi fupi sana (flash fiction) kwa mwaka 2014. Pia ni mwandishi was kitabu cha ushairi cha “See through the complicated” kilichotolewa mwakaa 2011. Neema ni mwanzilishi mwenza na mratibu wa La Poetista, ambayo hutoa nafasi kwa washairi na wasanii kwa ujumla, kuonesha vipaji vyao na kutumia sanaa yao kuleta athari chanya kwenye jamii. Pia ni mratibu wa “Woman Scream Festival” kwa Tanzania; tamasha la ushairi linalofanyika kote duniani kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake.

What's Your Reaction?
Excited
0
Happy
0
In Love
0
Not Sure
0
Silly
0
Scroll To Top
%d bloggers like this: