Now Reading
“Mgeni” by Fatma Shafii Mohamed

“Mgeni” by Fatma Shafii Mohamed

Usiku ulikuwa mwingi na utusi ukatanda kote. Kulikuwa na upepo mkali. Mvua ya kifuku ilinyesha mno huku radi zikipiga bila mpangilio. Sauti ya vyombo vikianguka vilisikika mara kwa mara. Madirisha yaliyoachwa wazi yalijibana na kujifungua kwa nguvu kupitia upepo huo. Tik tok tik tok, muda uliyoyoma. Binti huyo aliyekuwa kachoka hoi bin tiki alizuka kutoka katika malimwengu ya usingizi. Akanyanyuka na kuenda dirishani. Akazifungua pazia na kutizama nje. Halafu alirudi kitandani na kukaa huku amejifinika nusu mwili. Alitazama saa iliyoko pembeni mwa kitanda chake. Ilikuwa saa nane kasorobo. Alifotoka macho kwa mshangao. Akatazama nje tena. Kimya. Kichwa kilimzunguka kama tiara. Hofu ilimvaa. Alishika kitutu. Kwanini hajawasili? Aliwaza.

Ilikuwa tukizi sana kuchelewa namna hiyo. Alidhani huenda ikawa mvua nyingi hiyo ndio iliyomchelewesha.

Hapakulalika tena. Minghairi ya upepo huo, jasho lembamba lilimchirizika chiriri kwapani. Hakuelewa kabisa kilichoendelea. Alitoka chumbani kwake na kuenda kwa kaka yake. Kakaye alikuwa kalala fofofo. Alijaribu kumtikisa walau mara tatu, hakubanduka. Akaondoka na kuelekea mlipo na mlango wa chumba cha wazazi wake. Alisikia koromo kutoka alikosimama. Kumbe watu wote walikuwa wameshalala. Alirudi chumbani kwake.

Baada ya mda mrefu wa kumrai na kumueleza kuwa wakati mwafaka ulifika wa yeye kumtambulisha kwa wazazi wake, hatimaye alikubali. Na alfajiri ya kuamkia usiku huo ndio waliopanga kutimiza jambo hilo. Hamu ilimzidi kwani alitaka sana kuwaonyosha watu kuwa yeye ni mtu wa uhakika, na kuwa hakuwa akiwahadaa kuhusu mpenzi wake. Kuanzia na kaka yake, ambaye alikuwa akimchezea kila yaumu kuwa atazeekea nyumbani hadi kwa mama yake ambaye kila kukicha alimletea wanaume kutoka nasaba mbalimbali ili amuozeshe. Walakin, daima alikataa. Alikataa katakata na kuwaambia kuwa yupo ghulamu aliyetayari kumuoa na angemtambulisha hivi karibuni tu. 

Saa nane na nusu, bado hajatokeza. Aliona ni heri ajipurukushe na kujitayarisha ili kumpokea mpenzi wake, mumewe mtarajiwa. Aliamka akaingia bafuni na kukoga kwa maji ya fufutende na kuvaa mavazi aliali. Alivaa herini za fedha ambazo mpenziwe huzipenda na kuzisifu kila anapozifaa. Alipomaliza, alijirashia marashi ya mvuto mzuri. Kisha alisongeza kiti kinachokaa nyuma ya mlango na kukiweka karibu na kitanda chake. Kilikuwa hususan cha mgeni wake. 

Uhusiano wao ulikuwa wa mda sasa. Alikumbuka mara ya kwanza walipokutana. Saa tatu usiku, alipokuwa akikimbilia kununua padi dukani, kwani hedhi ilimtoka ghafla na hakukuwa na akiba ya padi yoyote nyumbani. Japo alikuwa na haraka ya kurudi, mwanamume huyo alimshinda nguvu na kupata kuongea naye kwa dakika chache. Na hivyo ndivyo polepole walikuja kujuana na kushikana zaidi. Mwanzomwanzo, alikuwa mwoga sana, asingethubutu kunena hata neno moja akiwepo naye. Lakini sasa walishazoeana, wangeliketi pamoja na kuongea huku wakicheka kufikia hadi kukumbatiana pindi anapomniadi. Matendo ya hivi karibuni ndio yaliyomzidisha mahaba kwake. Alianza kupapaswa nywele. Jambo ambalo hakuwahi kufanyiwa tangu apate fahamu zake. Wakaa mwengine, hushikwa mikono na kubusiwa viganja vyake. Isitoshe, zipo siku afikapo kuchelewa, basi maongezi yao huwa kalili na kuishia kupapaswa mgongo hadi kulala. Kuchelewa kwake hakukumtia dhiki, kwani alishamueleza kuwa afanyapo kazi, yeye ni mtu wa zamu ya jioni hadi usiku mwingi. Matendo haya yalileta hisia mpya kwake. Hisia iliyomuingia mpaka kwenye mishipa ya damu na kumfanya kusisimkwa na mwili mzima. Alifurahia. Usiku aliuona kuwa mchana na mchana kuwa usiku. Angalizubaa mchana kutwa tu akikumbuka matendo ya usiku uliopita au akiwaza atakachofanyiwa usiku utakaokuja. 

Alhasili, mashoga zake ndio waliokuwa na hamu zaidi ya kumuona mchumba huo, kwani ilikuwa kama wimbo wa taifa usio na ushuhuda. Kila kukicha angeliwaeleza namna ghulamu huyo alikuwa mfua uji, mwenye nywele zilizonyolewa kiufundi na masharafa kunyolewa mtindo wa shore. Ijapokuwa wapo waliomuamini walikuwepo wengine waliomuita mrongo na wegine kusema amechizika. Kilichowashangaza zaidi ni alipowaambia kuwa rijali huyo si wa kijiji hicho, bali hupitia njia anapokuwa akitoka kazini na kuelekea kwao, kijiji jirani. Walishangazwa na vipi angeweza kujuana na mvulana wa kijiji cha kando ilhali yeye mwenyewe hakuwahi kusafiri. Mara nyingi aliringa kwa kuwa aliamini mpenzi wake hakuwa shabaki kama walivyo wanaume wengi wa kijiji chao. Yote hayo yalikuwa fumbo kwao ambalo wakati pekee ndio ungelifumbua. 

Taibu, hayawi hayawi huwa yasiyokuwa yakawa. Saa tisa kamili. Mgeni aliyesuburiwa kwa raghba ya mkanja hatimaye aliwasili. Alimpokea mgeniwe huku amesheheni jazba isiyo ni mipaka. Alichachatika kwa furaha na bashasha. Roho yake iliyokuwa ikimdunda kwa wasiwasi sasa ulimdunda kwa furaha. Ndiyo, alijua asingekosa kuenda. Aliamini mapenzi aliyonayo kwake katu asingalivunja ahadi yake. Alimuamini sana rijali huyo.

Kama kawaida, mwanamume huyo alikaa kwenye kiti mkabala na alipo yeye kitandani. Halafu alimshika mikono na kubusu viganja vyake. Binti aliyeyuka. Akasahau wasiwasi wote aliomtia kabla afike. Akatabasamu.

“Laazizi akirami,” alinena mgeni, “Vipi hali yako?”

“Alhamdulillah, ” alijibu.

“Samahani sana kwa kuchelewa kufika leo. Kuna jambo lilitokea sikuwa na budi ila kulishughulikia, ”

“Jambo gani mpenzi?” 

“Mwenzangu wa kushika zamu baada ya mimi alipatikana udhuru nyumbani kwake hivi ilinilazimu niendelee kukaa kiasi cha yeye kufika,”

“Haina neno, almuradi umefika. Unajua leo ni siku yetu kubwa?”

“Nalifahamu hilo, ila… “

Akamkatiza, “Hapana mpenzi, leo sitaki sababu. Nilishamuahidi mama, kutakapombazuka leo nitakutambulisha kwake.” 

Alisimama na kuenda kwenye dirisha, huku akiangalia nje, alisema,

“Leo ni leo asemaye kesho ni mrongo. Siamini, hatimaye siku hii imefika. Nimesubiri mwia mrefu sana. Kweli, hakuna refu lisilo ncha. Watakoma kunichezea na kunisema. Eti mimi sipendeki. Chuoni wanasema mimi sio mrembo. Juzi tu nilisikia maskani wavlana wanasema mimi ni afkani. Kwanza ningependa kutazama sura ya kakangu utakapo kuwa unaongea na mama. Nimuone namna atakavyoshtuka. Haihalisi wao kutoniamini kabisa. Kwani nilikosea wapi?”

Alihisi kakumbatiwa kwa nyuma. Alianza kulia huku akitabasamu. Kisha alizunguka na kushika shavu la mpenziwe. Akamtazama ana kwa ana na kusema,

“Isitoshe, nahisi pia wakati umefika wa mimi kuolewa. Naamini nimekomaa kiakili na naweza kukuagalia vyema. Sitaki kuzeekea hapa wakati maswahiba zangu wanaolewa na kuzaa watoto. Ningependa unioe. Nina hamu sana. Unanipa raha na hauniudhi kama vile watu wengi wanifanyiavyo.”

Rijali alisongea karibu na uso wake na kumbusu kwenye bapa la uso. Walikumbatiana kwa mda. Halafu, walijibwaga kitandani na kujifunika. 

“Hivi ungependa harusi yetu tuifanye wapi?” alimuuliza mwanamume huyo.

“Kokote kule, nina hamu sana, sitaki shughuli ndefu. Ninataka nikuoe. Nikuchukue tuende tukaishi kule niliko mimi. Hutajuta. Nitakupa furaha isiyo na kifani”

“Wapi huko?”

“Kule kwetu, hakuna kuudhiana, hakuna kusumbuana, hakuna mwisho wa jambo, tutaishi milele, mimi na wewe tu.”

“Wacha masihara, kuna kitu kisicho mwisho kweli? Kila jambo lina mwisho wake. Mimi nataka niishi na wewe siku zote zilizobaki za maisha yangu”

Walicheka pamoja.

“Unajua nimekuwa nikiwaza bukrata wa ashiya. Kila nikikaa nawaza siku ya harusi yetu. Najua mama atafanya sherehe kubwa sana kwasababu mimi ndiye mwanae wa kike pekeyake. Halafu pia, yeye ni mama wa mtaa arifu sana. Harusi yetu itajaa mabalozi wa kila sehemu. Kijiji kitatemeka.” Alimalizia.

“Umewaza mbali mno” alimjibu.

Waliendelea kupiga soga huku wakioneshana mapenzi nao wasaa ukazidi kusonga. 

Liwike, lisiwike kutakucha! Alfajiri pevu ilijiri halafu majira ya asubuhi yalibisha hodi nalo jua tukufu likatapanya miale upeo wa macho na kuaga alfajiri. Mama mzazi alitoka chumbani na kuanza hamsini 

zake kama ilivyo ada ya nyumba hiyo. Alimtayarishia mumewe maji ya kukoga pamoja na kumuekea tauli bafuni. Alipomaliza, aliingia chumbani mwa mwanae wa kiume na kumwamsha huku akimhimiza kuwa kashachelewa kuswali swala ya alfajiri. Pilkapilka zikaanza. Moja baada ya mwingine alikuwa akiamka ila binti huyo.

“Hivi huyu kalala mpaka saa hizi? Hilo jua halimpigi chumbani?” aliuliza mama kwa sauti ya juu kana kwamba alikuwa anauliza watu wote mpaka majirani. Akaenda moja kwa moja hadi chumba cha bintiye 

na kufungua mlango.

“Surpriiiiiiiiiissseeeeee” alisema mwanae huku akitabasamu.

Alimuashiria mamake mkono kwa alipo laazizi wake.

“Mama kama nilivyokuahidi, kutana na mpenzi wangu. Tumekusubiri kwa hamu kuu uamke.”

“Mungu wangu!” alisema mama.

“Nilijua tu utashtuka, hata mimi binafsi natetemeka suala la kumtambulisha mpenzi wako kwa mzazi kumbe sio rahisi kama nilivyotarajiya,” 

Akatembea hadi alipo rijali huyo.

“My love, huyu ndiye nina 

yangu, kipenzi changu, mavyaa yako mtarajiwa. Songea basi, usiogope, hana shida yoyote.”

“Mwanangu! Hicho si kitanda tu?”

“Aaah maa please usianze masikhara, mie saa hii niko serious.”

“Mbona sioni mtu?”

“Mama, nahisi bado hujaamka vizuri,”

“Ya Ilahi!” alimaka mama, “hapana! Swaleheeee, we Swaleheee” 

“Naam,”aliitika barobaro aliyekuwa chumba mkabala na chumba hicho walichokuwa. 

“Hebu muite baba yako naona unga yamezidi maji huku”

“Kashaanza mambo yake?” Swaleh aliuliza.

“Tena leo kazidi, haraka muite huku,”

Binti huyo alianguka chini na kuanza kulia.

My Love, ongea. Umeona? Si nilikuambia hawatoniamini. Nimechoka. Nimechoka na maisha haya, ”

Alijibwaga chini na kulia kwa kwikwikwi huku machozi yakimtoka na kamasi zikimtona.


Fatma Shafi ni mwandishi wa kazi za kiswahili anayetoka pwani mwa Kenya. Anapenda kuandika kuhusu hulka za binadamu pamoja na maswali ibuka yanayoathiri bara la Afrika. Mashairi na hadithi zake zimewahi kuchapishwa katika majukwaa mbalimbali yakiwemo creativewritersleague.co.ke, Lolwe (An online literary magazine) na shiwaki.net. Ni mwanzilishi wa SHIWAKI, ambao ni Shirika la waandishi wa lugha ya kiswahili. Miongoni mwa kazi zake ni pamoja na hadithi fupi yake iliyomo ndani ya kitabu kiitwacho ‘Ndege Maji Ufukweni’,
kilichochapishwa katika lugha ya kifaransa, kiingereza English na Kiswahili baada ya kushinda shindano la Afro-Young Adult fiction. Pata kazi zake zaidi kupitia winowamarijani18.wordpress.com.

What's Your Reaction?
Excited
3
Happy
2
In Love
1
Not Sure
0
Silly
0
Scroll To Top

Discover more from Jalada Africa

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading