Now Reading
Mapinduzi ya Kutembea Wima

Mapinduzi ya Kutembea Wima

The Upright Revolution 4


Kiswahili

Idza Luhumyo

Hapo zamani, binadamu alitembea kwa mikono na miguu kama wanyama wengine walio na miguu minne. Alikwenda kwa kasi hata kuliko sungura, chui na kifaru. Kati ya viungo vyote vya mwili wa binadamu, ni miguu na mikono iliyokuwa na ushirikiano wa karibu zaidi. Ushirikiano huu ulitokana na kule kuwa na viungo ambavyo vililingana na kuambatana. Bega liliambatana na nyonga. Kiwiko kikajibiwa na goti. Kifundo cha mkono nacho kikawa sawia na kisigino. Wayo wa mguu ukawa unalingana na kofi la mkono, na viungo hivi viwili, yaani mikono na miguu, vilikuwa vyote na vidole vitanotano, kisha vikaishia kwa kucha. Mikono na miguu ilikuwa na mpangilio sawile wa vidole vitanotano kutoka kwa kidole gumba mpaka kwa kile kidole kidogo cha kando. Siku hizo, kidole gumba kilikuwa karibu na vile vidole vingine sawa tu na kile kidole kikubwa cha mguu. Basi ikawa miguu na mikono inaitana binamu kwa sababu ya uhusiano huu wao wa karibu.

Basi ikawa desturi ya mikono na miguu kusaidiana katika kuupeleka mwili popote ulipotaka kwenda; iwe sokoni, iwe madukani, ama hata kuikwea na kuishuka miti, milima na pahali popote pengine ambapo palihitaji mwendo. Hata mwili ulipokuwa majini, binamu wale walifanya kazi vyema kwa ushirikiano ili mwili upate kuelea, kuogelea ama kupiga mbizi. Uhusiano wao haukuwa na na ubaguzi wa aina yoyote. Walikuwa pia na ruhusa ya kuazima vipaji vya viungo vingine vya mwili kama vile sauti kutoka mdomoni, uwezo wa kusikia kutoka kwa sikio, uwezo wa kunusa kutoka puani na uwezo wa kuona kutoka kwa macho.

Kule kuelewana na kushirikiana kwa binamu hawa wawili kulivitia wivu viungo vingine vya mwili. Vikaanza kuchukizwa na tabia ya binamu wale ya kuazimaazima vipaji. Wivu huo ukaving’aza macho kiasi cha kuvifanya visahau kuwa kama si miguu na mikono, katu viungo vile havingeweza kutoka pahali pamoja na kwenda kwingine, na kisha kuondoka walipofika na kwenda kwengine. Vikaanza kupanga njama dhidi ya binamu wale.

Ulimi ukaazima njama kutoka kwa ubongo na kuitekeleza bila kupoteza wasaa. Kwa sauti ya juu, ulimi ukaanza kujadili kuhusu uwezo mkubwa waliokuwa nao binamu wale. Ulimi ulitaka kujua jambo moja: kati ya miguu na mikono, nani mwenye nguvu zaidi? Wale binamu wawili walikuwa kamwe hawajawahi kujihusisha na swala hilo. Ila sasa kila mmoja akaanza kusema kuwa yeye ndiye aliyekuwa muhimu katika mwili kuliko mwenzake. Jadiliano hilo likageuka upesi. Sasa ikawa swali la nani aliyekuwa muhimu kuliko mwenzake? Mikono ikawa ya kwanza kujipigia debe. Ikaanza kwa kusema kuwa vidole vyake vilikuwa vyembamba na vizuri, huku ikivikejeli vidole vya miguu kwa kuwa vifupi na vinono. Visiachwe nyuma, vidole vya miguu navyo vikavicheka vidole vya mikono kwa ule wembamba wao, vikawaita binamu wenye njaa! Basi majibizano yale yakaendelea kwa siku nyingi, hata yakaathiri kabisa ule ushirikiano ambao ulikuwepo zamani kati ya binamu wale wawili. Hatimaye, ilipobainika wazi kuwa kungekuwa na tatizo ikiwa jambo lile halingetatuliwa kwa haraka, binamu wale wawili wakaamua kuufikisha ugomvi wao mbele ya viungo vingine ili utatuliwe.

Ulimi ukatoa wazo: mbona kusiwe na mshindano ili kubaini swala hili? Viungo vyote vikakubaliana kuwa hilo halikuwa wazo baya. Lakini shida ilikuwa moja: mashindano yenyewe yapi haswa? Baadhi ya viungo vikatoa maoni, vikasema kuwe na mapigano ya mwereka kati ya miguu na mikono. Wengine walitaka kuwe na mapigano ya upanga, mauzauza, mbio za nyikani ama kucheza michezo mingine kama vile sataranji na drafu. Hatimaye mapendekezo yote hayo yalikataliwa kwani yangeleta utata wakati wa utekelezaji. Pia, walihofia ule uwezekano wa kuwepo ubaguzi. Basi ulimi ukaazima tena wazo kutoka kwa ubongo. Ukasema kuwa ulikuwa na suluhu mufti. Suluhu yenyewe ilikuwa hii: miguu ingechagua shindano la kuipa mikono nayo mikono ingechagua shindano la kuipa miguu. Wale binamu wakaridhika na wazo hili na wakalikubali.

Mashindano yalifanyika katika dawe lililokuwa msituni, karibu na mto mmoja. Ikabidi viungo vyote viwe machomacho ili viweze kuukinga mwili iwapo hatari yoyote ingejiri kwa sababu viungo vilikuwa vikipigana vita vya ndani kwa ndani. Macho yaliangaliaangalia huku na kule ili yapate kuona hatari yoyote ile; masikio yakawa tayari kusikia sauti yoyote; pua nayo ikajisafisha ili iweze kunusa hatari yoyote ambayo ingeyapita macho na masikio. Nao ulimi ukakaa tayari kupiga mayowe iwapo hatari yoyote ingetokea.

Upepo ukazipeperusha habari za mashindano yale katika pembe zote za msitu, maji na hewa. Wanyama wa miguu minne wakawa wa kwanza kukusanyika, wengi wao wakiyabeba matawi ya rangi ya kijani kibichi ili kuonyesha kuwa walikuja kwa amani. Basi mkusanyiko ule ukawa wa rangi rangile za wanyama tofauti tofauti kama chui, duma, simba, kifaru, fisi, twiga, ngamia, ng’ombe wa pembe ndefu, nyati, paa, swara, sungura, fuko na panya. Wanyama wa majini kama kiboko, samaki na mamba waliianika miili yao pale ufukweni, huku wakiziacha sehemu nyingine za miili yao ikiwa bado i majini. Wanyama wa miguu miwili nao hawakuachwa nyuma: mbuni, kuku na tausi wakayapigapiga mabawa yao kwa msisimko; ndege waliokuwa mitini wakaimba kwa uchangamfu ; chenene wakawa daima wakiimba. Buibui, minyoo, tandu na jongoo wakatambaa ardhini na mitini. Kinyonga naye alijikokota kwa utaratibu naye mjusi akawa anakimbiakimbia huku na kule. Nyani na sokwe wakawa wakirukaruka kutoka tawi moja hadi tawi lingine. Miti nayo ikayumbayumba katika upepo.

Mdomo ukayaanzisha mashindano yale kwa wimbo:

Twafanya haya tufurahi
Twafanya haya tufurahi
Twafanya haya tufurahi
Kwa kuwa sisi sote
Ni jamaa moja

Wale binamu, yaani mikono na miguu, wakaapa kuwa wangekubali matokeo ya mashindano bila kuzua ramsha au kutishia kuyagomea mashindano yale.

Mikono ilitoa shindano la kwanza. Walitafuta kigongo wakakirusha chini. Kisha wakasema kuwa kazi ya mguu ilikuwa moja tu: kukiokota kile kigongo na kisha baada ya hapo, kukitupa. Miguu ilikuwa na ruhusa ya kushauriana wakati wowote ule katika shindano, na pia ilikubaliwa kuvishirikisha vidole vyake ili kulitekeleza shindano lile. Basi miguu ikajaribu kukipindua kigongo kile, wakajaribu kukisukuma, wakazijaribu njia zote lakini wakashindwa kukiokota vizuri; na hata kule kukisongeza hakukuwa kwa mwanya, waliweza kukisukuma kwa hatua kidogo tu.

Vidole vya mikono kuona vile, vikaazima sauti kutoka kwa mdomo na vikaanza kucheka. Nayo mikono ikajitandaza na kujigamba kutokana na ule wembamba wao. Kisha wakakiokota kigongo kile kwa njia tofautitofauti. Wakakirusha mbali msituni na kuifanya halaiki kushusha pumzi kwa kuvutiwa na uhodari ule. Basi mikono ikaanza kuonyesha uhodari zaidi: waliviokota vipande vidogodogo vya mchanga kutoka bakuli la mchele; wakapitisha nyuzi sindanoni, wakatengeneza kapi ndogo za kusukuma magogo mazito, wakaunda mishale na kuirusha mbali. Miguu kamwe haingeweza kutenda vitendo hivi, labda ndotoni. Basi miguu ikaduwazwa kwa ule ustadi wa binamu wao wakonde. Halaiki ikapiga makofi kwa nguvu ili kuonyesha dhahiri ujamaa kati ya mikono yao na ile mikono ambayo ilikuwa ikitekeleza shindano kwa wakati ule. Jambo hili liliikera sana miguu. Ingawa miguu ilionekana kuwa yenye udhoofu, kamwe haikukata tamaa. Vidole vya miguu vilitapatapa mchangani katika pilka za kutafuta shindano la kuwapa binamu wao.

Basi hatimaye ikawa zamu ya miguu kuipatia mikono shindano. Ilisisitiza kuwa haikuwa na mengi. Ilitaka mikono iubebe mwili wote kutoka sehemu moja ya duara mpaka sehemu nyingine. Vidole vya mikono vikajibu kwa kiburi kuwa hilo lilikuwa shindano la kipuzi kweli!

Ikawa sinema. Mwili ukapinduka juu-chini. Mikono ikawa kwenye ardhi nayo miguu ikaelea angani. Macho yakajipata mchangani yasiweze tena kuona vyema, na pua ikachemua kwa ajili ya vumbi.

Halaiki ikaanza mayowe na kuimba:

Nyayo Nyayo juu
Hakuna matata
Fuata nyayo
Hakuna matata
Turukeni angani

Halaiki ilielekeza macho yao kwenye mikono. Muda mchache tu uliopita, mikono ilikuwa imeonyesha umahiri lakini sasa ilikuwa dhaifu mno. Ilipiga hatua kidogo, kisha ikalia kwa uchungu, ikachechemea, na kuuacha mwili uanguke. Ikapumzika, na kujaribu tena. Safari hii, mikono ilijaribu kuvitawanya vidole ili iweze kuushikilia mwili vizuri ila ni vidole gumba tu ambavyo viliweza kuvutika. Ikajaribu kupinduka kichwa-gomba lakini ujanja huu wao ukakataliwa kwa kuwa ungehitaji usaidizi wa miguu.

Basi ikawa zamu ya vidole vya miguu kucheka. Vikaazima sauti nzito ya kutoka kooni ili wakitofautisha kicheko chao na kile cha vidole vya mikono. Kejeli ile ikaichukiza mikono na basi ikajaribu mara ya mwisho kuubeba mwili. Ikashindwa kusonga hata hatua moja. Uchovu uliizidi na basi ikakata tamaa. Miguu nayo haikupoteza muda kuonyesha ustadi wao. Ikajipigapiga chini kutumia nyayo zao, ikaanza kusongea, kasha ikakimbia, na kuruka. Miguu ilitenda vitendo hivi vyote bila kuuacha mwili uanguke hata mara moja. Nayo miguu yote ya halaiki iliyokusanyika ikazipigapiga nyayo zao chini ili kuonyesha umoja wao na miguu ya mwili. Mikono ilijaribu kukipinga kitendo hiki, huku ikiwa imesahau kuwa hiyo ndiyo iliyotangulia kuikejeli miguu.

Lakini jambo moja likawa dhahiri: vile vidole gumba vilivyojivuta katika ile harakati ya shindano vilibaki vikiwa kando ya vile vidole vingine. Halaiki ilianza tena kucheka lakini kicheko chao kikapungua walipogundua jambo lingine: kile kidole cha gumba kilichokuwa kando ya vidole vingine hakikiufanya mkono uwe na kilema bali kiliufanya mkono uweze hata kuifanya kazi vizuri zaidi. Mambo gani haya? Yaani leo kilema kimekuwa kitu cha kushangiliwa!

Basi mjadala wa nani mshindi wa mashindano yale ukaendelea kwa muda wa siku tano, sawia na idadi ya vidole iliokuwa kwenye kila kofi na kwenye kila wayo. Lakini hawakuweza kuamua nani mshindi, kwa kuwa kila mmoja wao alikuwa na uhodari wake maalum, na pia kwa kuwa kila binamu alimtegemea mwenzake.

Kikao cha falsafa kikatokea. Swala kuu: nini hasa ndicho kiini cha mwili? Hatimaye ikabainika kuwa kiini chenyewe kilikuwa jumla ya viungo vyote vikishirikiana. Ili kuhakikisha kuwa ugomvi wa namna ile haungetokea tena, na pia ili kuhakikisha kuwa viungo vyote vya mwili vingeweza kutekeleza majukumu yao bila kuhitilafiana, wakaamua kuwa mwili ungetembea wima, miguu ikiwa chini huku mikono ikilewalewa hewani. Suluhu hii ikawaridhisha ila tu ilibainika kuwa ni sharti watoto watambae ili wasiisahau asili yao.

Wakagawanya kazi: miguu ingeusafirisha mwili, kisha mikono ingechapa kazi na kuvishika vifaa. Huku miguu ikitekeleza kazi nzito ya kuusafirisha mwili, mikono ingetumia kipawa chao kufanya kazi katika mazingira, na kuhakikisha kwamba chakula kilifika mdomoni. Mdomo, au meno haswa, ungetafuna chakula hicho na kukipitisha kooni mpaka kukifikisha tumboni. Tumbo nalo lingechukua virutubisho vyote kwenye chakula hicho na kukipitisha kwenye mabomba yake ili manufaa ya chakula hicho yaenee katika sehemu zote za mwili. Kisha tumbo lingetupa mabaki kwenye mitaro ya mwili ili uchafu huo uweze kutumbukizwa madaweni au kufukiwa ardhini ambamo yangenufaisha mimea. Nayo mikono ingeyachuma matunda kutoka kwenye mimea kabla ya kuitia mdomoni. Aha! Mviringo wa maisha huo.

Hata hivyo, ilikuwa dhahiri kuwa mpangilio huu bado ulikuwa na uwezo wa kuzua utata baadaye. Kwa kuwa kichwa kilielea juu, huenda kikadhani kuwa kilikuwa bora zaidi kuliko miguu iliobaki ardhini. Pia, huenda kikadhani kuwa mamlaka yote yalikuwa yake. Ikawa muhimu sana kusisitiza ule usawa baina ya viungo vyote ili raha kwa mmoja iwe ni raha kwa wote, na uchungu kwa mmoja uwe uchungu kwa wote . Viungo vikaukanya mdomo na kuuambia kuwa uliposema “changu” au “kile changu” uliongea kwa niaba ya mwili mzima.

Wakaimba:

Mwilini mwetu
Hakuna mtumishi
Mwilini mwetu
Hakuna mtumishi
Tunatumikiana
Sisi kwa sisi
Tunatumikiana
Ulimi ni sauti yetu
Nibebe nami nikubebe
Tuujenge mwili wenye afya
Nishike nikushike
Tujenge mwili wenye afya
Uzuri ni umoja

Twafanya kazi pamoja
Ili tuwe wenye afya
Twafanya kazi pamoja
Kuupata mwili wenye afya
Umoja ni nguvu yetu

Huu ukawa wimbo maalum wa mwili. Nao mwili unauimba wimbo huu mpaka siku ya leo. Na hivi ndivyo wanadamu na wanyama wanavyotofautiana. Wanyama walikataa kujihusisha na mapinduzi ya kutembea wima.

Laiti ya waliyoyashuhudia, wanyama kamwe hawakutaka kujishirikisha na mapinduzi hayo. Hilo jambo la kuimbaimba waliliona kuwa la kipuzi sana. Waliona kuwa kazi ya mdomo ni moja na kazi yenyewe ni kula, si kuimba! Basi wakakiunda chama chao cha kuyakataa mapinduzi.

~
Edited by Okwiri Oduor
~
Read the English translation – The Upright Revolution: Or Why Humans Walk Upright by Ngugi wa Thiong’o


Idza Luhumyo is a writer-becoming, a lawyer-becoming and a woman-becoming. She is a founding member of Jalada African Writers’ collective.

What's Your Reaction?
Excited
0
Happy
0
In Love
0
Not Sure
0
Silly
0
Scroll To Top